Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema kuwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amempigia simu na kumwambia kuwa ana imani naye na kuwa hajafikiria kutengua uteuzi wake labda kumpandisha cheo.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya taarifa kuhusu Rais kutengua uteuzi wake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa alipigiwa simu nyingi na watu wengi lakini kabla hajawajibu Rais Magufuli akampigia simu na kumueleza kuwa ana imani naye na kuwa ahakikishe anawatumikia wananchi wa Arusha kwani yeye sio bosi wao bali ni mtumishi wao.
Pia mkuu wa mkoa alieleza kuwa Rais amempa maagizo ya kuhakikisha anasimamia wananchi wa mkoa wa Arusha walipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya mkoa huo na nchi kwa ujumla.
Aidha, ili kuthibitisha kuwa ni Rais Magufuli ndiye aliyempigia simu, Rais aliomba kuongea na yeyote aliyekuwa karibu ndipo mkuu wa mkoa akampa mmoja wa waliokuwa katika mkutano huo kuthibitisha kuwa ni Rais Magufuli.
Habari ya kutenguliwa kwa mkuu wa mkoa wa Arusha imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kuibuka mvutano mkali kati ya mkuu huyo wa mkoa na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kuhusu mradi wa ujenzi wa hospitali itakayotoa huduma kwa mama na mtoto mkoani humo.