Lowassa na Kikwete Wakutana Uso Kwa Uso Dar - HABARI TANZANIA

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Tuesday, 18 October 2016

Lowassa na Kikwete Wakutana Uso Kwa Uso Dar


Hatimaye mazishi ya kuuaga mwili wa Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam,Dk. Didas Masaburi, yamewakutanisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassana Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kwa kusalimiana na kushikana mikono.

Tukio hilo la aina yake liliwafanya watu mbalimbali waliokuwa katika msiba huo kubaki wakishangaa, hasa baada ya Rais mstaafu Kikwete kumfuata Lowassa na kumwuliza hali rafiki yake huyo wa zamani waliokulia wote CCM.

Tangu wakati huo viongozi hao ambao walikuwa marafiki wa karibu tangu ujana wao walikuwa wakirushiana vijembe ambapo jana walikutana ana kwa ana katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wa kuuaga mwili wa Dk. Masaburi kabla ya kwenda kuzikwa nyumbani kwake Chanika Manispaa ya Ilala.

Akiwa katika viwanja hivyo, Kikwete alipomwona Lowassa akiingia viwanjani hapo alinyanyuka na kumfuta Lowassa katika kiti chake kisha kusalimiana naye kwa kupeana mikoni huku wakizungumza.

Lowassa aliyekuwa ameketi jirani na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na mkewe Regina Lowassa, alisimama na kumjibu salamu.

Kwa muda mrefu wanasiasa hao ambao wamewahi kuwa marafiki hadi kupewa jina la utani ‘Boys II Men’, waliingia katika uhasama kwa kile kinachodaiwa ni kusalitiana kisiasa.

Urafiki wa wawili hao ulianza kuingia doa mwaka 2008 wakati wa kashfa ya Richmond iliyosababisha Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa kile alichoeleza ni kunyimwa haki ya kusikilizwa baada ya kuibuka kwa kashfa hiyo kwa kile alichodai ilikuwa ni vita ya kutaka ‘uwaziri mkuu’.

Ukaribu wa Lowassa na Kikwete uliendelea kupungua na kuwa shakani zaidi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana baada ya Lowassa kukatwa jina lake katika kinyang’ anyiro cha kuwania nafasi ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuamua kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kwa takribani mwaka mmoja sasa tangu mchakato wa ndani wa CCM wa kumpata mgombea wake wa urais Julai 10, mwaka jana umalizike wawili hao hawajawahi kukutana hadharani na kupeana mikono.

Katika mchakato huo Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa manane iliibuka na jibu kwamba, jina la Edward Lowassa limekatwa katika watu wanaowania urais kupitia chama hicho.

Waliopitishwa na kuingia tano bora na Kamati Kuu walikuwa ni Bernard Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali, huku makada wengine 33 wakitupwa akiwamo Lowassa.

Kutokana na hali hiyo Lowassa alichukua aumuzi mzito wa kuihama CCM, Julai 28, mwaka jana na kujiunga na Chadema na hatimaye kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho cha upinzani akiungwa mkoano na vyama vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here